IQNA

Utawala wa Myanmar wabomoa misikiti 16 katika jimbo la Rakhine

15:31 - December 13, 2017
Habari ID: 3471308
TEHRAN (IQNA)-Utawala wa Kibuddha wa Myanmar umebomoa misikiti 16 kati ya 17 katika vijivi vya eneo Haindafar katika jimbo la Rakhine lenye Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Taarifa zinasema vijiji vya eneo la Haindafara vimekuwa vikishambuliwa vikali tokea mwezi Agosti wakati jeshi la nchi hiyo lilipoanzisha wimbi jipya la hujuma dhidi ya Waislamu.

Walioshuhudia wanasema mwishoni mwa mwezi Novemba misikiti hiyo ilibomolewa katika hujuma iliyotekelezwa na mabuldoza ya jeshi la nchi hiyo. Aidha nyumba za Waisalmu katika eneo hilo pia zimeteketezwa moto katika oparesheni hiyo.

"Baada ya kuteketeza nyumba zetu, serikali sasa inalenga maeneo yetu ya ibada," amesema mwanakijiji moja aliyejawa na majonzi. Hivi sasa wanakijiji wana hofu kuwa msikiti uliobakia utabomolewa  na wala hawana uwezo wa kuzuia jinai hiyo. Makumi ya misikiti tayari imeshambomolewa katika wimbi jipya la hujuma ya wanajeshi na mabudhha wenye misimamo ya kufurutu adha dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Jinai kubwa wanazofanyiwa Waislamu hao na wanajeshi na Mabudha wa nchi hiyo  wenye misimamo ya kufurutu katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa Myanmar  tangu tarehe 25 mwezi Agosti mwaka huu; hadi sasa zimepelekea kuuliwa Waislamu zaidi ya elfu sita na kujeruhiwa maelfu ya wengine huku zaidi ya laki sita wakilazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Wiki iliyopita Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Zeid Ra'ad Al Hussein alisisitiza katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lililokutana kujadili hali ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine huko Myanmar kwamba, kuna udharura wa kufika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kufanya uchunguzi kuhusu ukatili unaofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa kutotambua haki za watu wa jamii ya Rohingya kama kaumu yenye haki na heshima ni kuwadunisha na kuwadhalilisha Waislamu wa Myanmar.

Ra'ad Al Hussein amesema kuwa, Waislamu wa Rohingya wanalengwa na kuuawa kwa sababu ya utambulisho wao na kwamba wananyimwa hata haki ya kuwa na majina ya Kiislamu.

3464685

captcha