IQNA

Misikiti Uingereza yawapokea wasio na makao katika msimu wa baridi kali

21:29 - March 03, 2018
Habari ID: 3471414
TEHRAN (IQNA)-Misikiti kadhaa nchini Uingereza imefungua milango kwa watu wasio na makao nchini humo bila kujali dini yao kufuatia baridi kali na theluji iliyovunja rekodi nchini humo na kupelekea watu zaidi ya 11 kupoteza maisha katika kipindi cha wiki moja.

Misikiti Uingereza yawapokea wasio na makao katika msimu wa baridi kali

Siku ya Ijumaa Idara ya Hali ya Hewa Uingereza ilitoa tahadhari ya juu zaidi ya theluji katika maeneo la kusini magharibi mwa England na kusini mwa Wales. Theluji hiyo kali iliandamana na upepo na hivyo kupelekea hali kuwa mbaya kwa maelfu ya watu ambao hawana makao uingereza.

Kufuatia hali hiyo, misikiti kadhaa kote Uingereza imewapa hifadhi na chakula watu hao. Kwa mfano Msikiti wa Makii Masjid katika mji wa Manchester umetoa huduma kwa idadi kubwa ya watu wasio na makao mjini humo. Rabnawaz Akbar, mwanakamati katika msikiti huo anasema: “Baridi imekuwa kali sana na hivyo tumeamua kuwasaidia wasio na makao.” Waislamu waliojitolea wamekuwa wakitoa huduma mbali mbali kwa watu hao  katika msikiti huo. Misikiti mingine iliyofungua milango yake kutoa huduma katika kipindi hiki ni pamoja na Msikiti wa Jamia wa Leeds, Msikiti wa Oldham, Msikiti wa Finsbury Park, Msikiti wa Canterbury. Aidha katika nchi jirani ya Ireland, Msikiti wa Clonskeage mjini Dublin umefungua milango yake kwa wasiokuwa na makao ili kuwanusuru kutoka baridi kali.

Imamu wa Msikiti wa Oldham ambao unasimamiwa na Kituo cha Kiislamu cha Ulaya (EIC) Sheikh Mohammed Iqba anasema awali waliwapa misaada ya nguo watu wasio na makao lakini ikabainika kuwa kutokana na baridi kali sana wanahitaji sehemu ya kulala na kwa msingi huo wakapewa hifadhi ndani ya msikiti. Amesema baridi yam waka huu imevunja rekodi na kwa msingi huo msikiti huo unawapa hifadhi watu karibu 15 wasio na makao.

Baridi kali barani Ulaya, ambayo imesababishwa na wimbi la baridi kutoka maeneo ya Siberia, Russia, imesababisha vifo vya watu 11 Uingereza. Upepo mkali wa baridi, ambao umepewa jina 'Nduli kutoka Mashariki' nchini Uingereza, unavuma kote barani, na viwango vya joto vimeshuka hadi nyuzi -30C.

3465306

captcha