IQNA

Rais Hassan Rouhani wa Iran

Ukombozi wa Quds ni Lengo Takatifu la Taifa la Iran na Waislamu wote

22:28 - June 07, 2018
Habari ID: 3471546
TEHRAN (IQNA)- Rais Hassan Rouhani amesema: Siku ya Quds ni siku ya kihistoria ya kupaza mayowe dhidi ya madhalimu na kulihami taifa linalodhulumiwa ambalo kwa muda wote wa miaka 70, watu wake wamehamishwa kidhulma kwenye nyumba na makazi yao.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo kupitia ujumbe aliotoa kwa mnasaba wa kuwadia Siku ya Kimataifa ya Quds. Huku akikumbusha kuwa Siku ya Quds ya mwaka huu ina hali na mazingira maalumu, Rais Rouhani amesema: Mbali na mwaka huu kutimia miaka 70 tangu kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina, tumeshuhudia pia jinsi Marekani ilivyokiuka na kudharau kanuni na sheria zote za kimataifa kwa kuitambua rasmi Baitul Muqaddas, ardhi inayoheshimika mbele ya Waislamu wote, kuwa mji mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa: Mwaka huu pia dhulma na jinai kubwa zaidi zimezidi kuwaandama Wapalestina madhulumu hasa wa Ukanda wa Gaza; na kwa upande mwingine katika miezi iliyopita tumeshuhudia jinsi viongozi wa utawala wa Kizayuni walivyozidi kuhaha huku na kule ili kueneza hofu na chuki dhidi ya Iran na kutaka kuyadhuru maslahi ya taifa kubwa la Iran.

Rouhani amesisitiza kwamba: Kwa kushiriki wote pamoja katika maandamano makubwa ya Siku ya Quds, wananchi wa Iran wataufikishia ujumbe utawala ghasibu wa Kizayuni kwamba bado hawajaisahau Palestina na Quds tukufu; na ukombozi wa Quds tukufu lingali ni tamanio na tarajio takatifu kwa taifa la Iran na Waislamu wote duniani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha pia kwamba haiko mbali siku ambapo wananchi wa Palestina watarejea kwenye nyumba na makazi yao, na Waislamu wataweza kusali Baitul Muqaddas, kilipo kibla chao cha kwanza.

Maandamano ya Siku ya Quds ya mwaka huu yatafanyika hapa nchini Iran na katika nchi zingine duniani Ijumaa ya kesho tarehe 8 Juni itakayosadifiana na tarehe 23 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani,

Ikumbukwe kuwa kufuatia ubunifu wa Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ilitangazwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds. Katika siku hii Waislamu na wapenda haki kote duniani hujumuika ili kubainisha kuchukizwa kwao na sera za kibaguzi za utawala wa Kizayuni wa Israel huku wakitangaza kuunga mkono malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina. Wapalestina wanapigania ukombozi wao kwa lengo la kuunda nchini huru ya Palestina, mji wake mkuu ukiwa ni Quds (Jerusalem) Tukufu.

3720758/

captcha