IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Palestina ni kadhia ya kwanza na muhimu kabisa katika Ulimwengu wa Kiislamu.

19:51 - July 22, 2019
Habari ID: 3472053
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, ushindi haupatikani bila ya muqawama na mapambano na kwa mujibu wa ahadi isiyo na shaka ya Mwenyezi Mungu, hatima ya kadhia ya Palestina bila shaka itakuwa ni kwa manufaa ya Wapalestina.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesema hayo leo mjini Tehran alipokutana na ujumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ambapo amebainisha kwamba, Palestina ni kadhia ya kwanza na muhimu kabisa katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ni kitovu cha harakati huko Palestina kama ambavyo Palestina ni kitovu cha harakati katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Ayatullah Ali Khamenei ameeleza kuwa, kusimama kidete wananchi wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni bishara ya ushindi na akaongeza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina muhali wala kuionea haya nchi yoyote ile duniani kuhusiana na kadhia ya Palestina, kwani kuiunga mkono Palestina ni suala la kiitikadi na kidini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema pia kuwa, hatua ya kujiweka mbali na kadhia ya Palestina baadhi ya nchi zinazoifuata Marekani kama Saudi Arabia ilikuwa ni ujinga, kwani kama zingeliiunga mkono Palestina hatua hiyo ingekuwa ni karata ya turufu kwao mkabala na Marekani.

Ayatullah Khamenei ameashiria mpango wa kiusaliti wa 'Muamala wa Karne' na kusisitiza kwamba: Lengo la mpango huu hatari ni kutokomeza utambulisho wa Palestina baina ya wananchi na vijana wa Kipalestina ambapo haipaswi kuwaruhusu Wamarekani wasambaratishe utambulisho wa Palestina kwa kutumia fedha.

3829099

captcha