IQNA

Rais wa Ufaransa apinga vazi la Hijabu katika idara za umma

21:25 - October 25, 2019
Habari ID: 3472186
TEHRAN (IQNA) – Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameendelea sera zake za chuki dhidi ya Uislamu kwa kusema anapinga vazi la staha la Hijabu la wanawake Waislamu kuvaliwa katika idara au taasisi za kiserikali zinazotoa huduma kwa umma.

Akizungumza katika kisiwa cha Re Union Alhamisi, Macron amesema hajali iwapo wanawake Waislamu wanavaa hijabu katika sehemu za umma au hadharani lakini anapinga wafanyakazi wa idara au taasisi za kiserikali kuvaa Hijabu. Rais wa Ufaransa amesema hasa anapinga vazi la Hijabu katika shule za serikali.

Macron ametoa kauli hiyo kumjibu Marine Le Pen, kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia chenye misimamo ya kibaguzi cha Rassemblement National, ambaye ametaka Hijabu ipigwe marufuku katika maeneo yote ya Umma Ufaransa.

Rais Macron amekuwa akitekeleza sera  kuzuia harakati za Waislamu nchini Ufaransa na kuwawekea mipaka kama vile kuzuia vazi la Hijabu kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa Kiislamu. Hivi karibuni Ahmet Orgas, mkuu wa Baraza la Waislamu wa Ufaransa (CFCM) ameonya juu ya nia mbaya iliyo nyuma ya pazia ya Emmanuel Macron kuwalenga Waislamu.

Kadhalika Ahmet Orgas, amelaani vikali vita vya vyombo vya habari kuilenga dini ya Kiislamu na Waislamu nchini humo. Kuna takribani Waislamu milioni tano Ufaransa wengi wao wakiwa ni wahamiaji kutoka nchi za kaskazini mwa Afrika na idadi hiyo ni takribani asilimia nane ya Wafaransa wote.

3852367

captcha