IQNA

Waislamu waomboleza katika kumbukumbu ya kuaga dunia Mtume Muhammad SAW

17:32 - October 27, 2019
Habari ID: 3472189
TEHRAN (IQNA) Waislamu leo wako katika maomboleo, simanzi na huzuni kubwa kwa mnasaba wa kukumbuka tukio chungu zaidi ya yote la kuaga dunia mbora wa Mitume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad bin Abdullah SAW

Kwa mnasaba wa siku ya leo tarehe 28 Mfunguo Tano Safar tangu jana jioni maeneo katika nchi nyingi za Kiislamu ikiwemo Iran na maeneo mengine duniani Waislamu walijumuika katika kukumbuka tukio la kuaga dunia Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad SAW na mjukuu wake, Hassan bin Ali bin Abi Twalib AS aliyeuawa shahidi katika siku kama hii ya leo. 

Misikiti, Husainiya (kumbi za kidini) na kumbi nyingi za masuala ya kijamii tangu jana jioni zilifurika waumini wenye huzuni waliokwenda kusikiliza hotuba, mashairi na tungo za kumsifu Mtume Muhammad SAW na Ahlibaiti zake na kueleza mengi yaliyofanywa na Mtukufu huyo kwa ajili ya kuwaondoa wanadamu kwenye giza na kuwaingiza kwenye nuru na dini ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu. 

Nchini Iran, shughuli kama hiyo ambazo zilifika kileleni leo tarehe 28 Safar zinashuhudiwa zaidi katika miji mitakatifu ya Mash'had na Qum ambako mamilioni ya Waislamu wanakusanyika katika haram za wajukuu wa Mtume SAW kudhihirisha mapenzi yao kwa watukufu hao na kuonesha mshikamano wao mkubwa na mafundisho ya Nabii Muhammad, rehma na amani za Allah ziwe juu yake na Aali zake. 

Mtume Muhammad SAW alifariki dunia siku kama ya leo tarehe 28 Safar mwaka wa 11 Hijria akiwa na umri wa miaka 63.

Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Mtukufu SAW alipata umashuhuri kwa jina la "Muhammad Mwaminifu". Akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SW alimteua kuwa Mtume Wake ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga. 

3469746

captcha