IQNA

Warsha ya Qur'ani kuhusu kupambana na ugaidi yafanyika Misri

16:44 - November 02, 2019
Habari ID: 3472197
TEHRAN (IQNA)-Chuo Kikuu cha Cairo nchini Misri kimeandaa warsha iliyojadili mada ya 'Vita Dhidi ya Ugaidi Kwa Mtazamo wa Qur'ani'.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, warsha hiyo imefanyika Oktoba 29 katika Kitivo cha Darul Ulum cha Chuo Kikuu cha Cairo na kuhudhuriwa na waalimu pamoja na watafiti  wa Chuo Kikuu cha Al Azhar. Aidha waandishi habari kutoka vituo vya televisheni na magazeti wameshiriki katika warsha hiyo.

Lengo kuu la warsha hiyo limetajwa kuwa ni kusisitiza kuhusu haja ya kutekeleza mafundisho ya Qur'ani na kusambaza fikra za amani, uadilifu na uhuru kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu.

Taarifa ya mwisho ya warsha hiyo ilisomwa na Osama Ibrahim al Amin, mwandishi habari wa Misri ambaye ni katibu mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Ujumbe wa Amani ambapo washiriki walisisitiza kuhusu ulazima wa kukabiliana na itikadi potovu ambazo zinaenezwa kwa jina la Uislamu.

Aidha taarifa hiyo imesisitiza kuhusu kutegemea Qur'ani Tukufu kama marejo asili ya Uislamu na kutumia aya zake kwa ajili ya kuligania amani, rehema, uadilifu, uhuru, urafiki na kuheshimiana. Halikadhalika warsha hiyo imetilia mkazo ulazima kwa kurekebisha mitaala ya vyuo vya kidini na madrassah huku Chuo Kikuu cha Al Azhar kikitakiwa kuimarisha mikakati ya kueneza utamaduni wa kutumia mantiki miongoni mwa Waislamu duniani.

3853515

captcha