IQNA

Wapinzani Bahrain walaani hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi Sheikh Ali Salman

21:38 - November 06, 2019
Habari ID: 3472203
TEHRAN (IQNA)- Chama kikuu cha upinzani cha Bahrain, Al Wefaq, kimelaani kutolewa hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya kiongozi wake, Sheikh Ali Salman.

Taarifa iliyotolewa na Al Wefaq imesema  Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu zimehusika katika kutolewa hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya Sheikh Ali Salman.

Aidha taarifa hiyo ambayo imetolewa kwa munasaba wa kutimia mwaka moja tangu itolewe hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya Sheikh Ali Salman  imesema vyombo vya mahkama vya Bahrain havifanyi kazi kwa uhuru bali vinafuata matakwa ya utawala wa kidikteta wa Aal-Khalifa.

Al Wefaq imeongeza kwamba, hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya mwanazuoni huyo na kiongozi wa kisiasa nchini Bahrain pamoja na manaibu wake wawili, Hassan Sultan and Ali al-Aswad, ilitolewa katika anga ya ukosefu wa uadilifu wa vyombo vya mahakama na kutokuwepo usawa wa kisheria nchini humo. Tarehe 24 Oktoba 2018 utawala wa Aal Khalifa ulimuhukumu kifungo cha maisha jela Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Al Wefaq na Sheikh Hassan Sultan pamoja na Ali Al-Aswad, ambao ni wabunge wa zamani wa bunge la nchi hiyo kwa tuhuma bandia eti za kuifanyia ujasusi Qatar. Sheikh Ali Salman alitiwa mbaroni mwaka 2014.

Tangu Februari mwaka 2011, wakati ulipoanza mwamko wa Kiisamu Asia Magharibi, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, utekelezwe uadilifu, ukomeshwe ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.

Hata hivyo kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati waliotumwa nchini Bahrain kupitia mpango wa ulinzi wa Ngao ya Kisiwa, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kukabiliana na matakwa ya wananchi hao.

Kwa mujibu wa duru za haki za binadamu, Bahrain ina idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa kulinganisha na idadi ya watu katika nchi hiyo ndogo zaidi katika Ghuba ya Uajemi.

3469819

captcha