IQNA

Uchumi wa Somalia waathiriwa vibaya na kupungua mahujaji

22:45 - August 01, 2020
Habari ID: 3473022
TEHRAN (IQNA) – Kupunguzwa kwa kiasi kikubwa idadi ya Waislamu waliotekeleza ibada ya Hija mwaka huu kumeathiria vibaya sana uchumi wa Somalia ambapo hutegemea uuzaji wa mamilioni ya mifugo nchini Saudia wakati wa Hija.

Kwa mujibu wa takwimu mahujaji mwaka huu hawakuzidi 10,000 katika hali ambayo katika miaka ya hivi karibuni idadi hiyo imekuwa ni milioni mbili na nusu. Mahujaji ambao hufika Makka  kila mmoja huchinja ima mbuzi, kondoo, ngamia au ng’ombe na kwa msingi huo kupungua mahujaji kunamaanisha kupungua kwa kiasi kikubwa mifugo iliyochinjwa.

“Biashara ni mbaya,” amesema Yahye Hassan anayefanya kazi katika soko la mifugo katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. “Athari mbya za janga la corona zinahisika,” ameongeza Hassan na kubaini kuwa, “nchi za Kiarabu hazihitajii mifugo kutoka Somalia. Wafugaji ambao huleta mifugo nao pia hawataki kufika Mogadishu wakihofia kuambukizwa corona.”

Saudia hununua karibu thuluthi tatu ya mifugo yote ya Somalia ambayo huuzwa nje ya nchi. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, mwaka 2015, Somalia iliiuzia Saudia mifugo zaidi ya milioni tano wakiwemo kondoo, mbuzi, ngamo na ng’ombe.

Hivi sasa bei ya mifugo imeshuka sana Somalia kutokana na kupungua uuzaji nje ya nchi. Kwa mfano ngamia ambaye hugharimu dola elfu moja sasa anauzwa kwa dola mia tano.

3472150

captcha