IQNA

Kiongozi Muadhamu atume ujumbe wa rambi rambi kufuatia mlipuko wa Beirut

17:15 - August 06, 2020
Habari ID: 3473039
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe kufuatia tukio la mlipuko katika bandari ya Beirut nchini Lebanon na kutangaza kuwa pamoja na serikali na wananchi wa nchi hiyo katika kipindi hiki kigumu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema katika ujumbe wake wa Twitter ulienezwa na mtandao wa Khamenei.ir siku ya Jumatano kwamba: Tuko pamoja na wananchi wapendwa wa Lebanon kufuatia tukio hilo chungu la mlipuko ambalo limesababisha kufariki dunia watu wengi pamoja na kusababisha hasara kubwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kuwa na subira mbele ya tukio hili kutaandika historia nzuri kwa taifa la Lebanon.

Katika mlipuko mkubwa uliotokea Jumanne usiku katika mji mkuu wa Lebanon  Beirut zaidi ya watu 100 waliuawa na wengine wasiopungua 4000 kujeruhiwa.

Mlipuko huo ulitokea katika ghala nambari 12 la Bandari ya Beirut na kwamba sababu ya moto ni mada za milipuko ambazo zilikuwa zimehifadhiwa hapo.

Mlipuko huo ulikuwa mkubwa kiasi cha kusikika kilomita nyingi kutoka eneo la tukio. Taarifa zaidi kutoka mji mkuu wa Lebanon Beirut zinasema kuwa, mlipuko huo umesababisha hasara kubwa kwa nyumba za makazi na pia katika idara binafsi na za serikali hasa majengo yaliyokuwa karibu na tukio hilo.

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, zaidi ya watu 300,000 wamebaki bila makazi mjini Beirut baada ya nyumba zao kuharibiwa kabisa na mlipuko huo.

Wakati huo huo, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa serikali na taifa la Iran litaendelea kuwa pamoja na watu wa Lebanon kama ilivyokuwa siku zote na kuongeza kuwa, taifa kubwa la Lebanon litavuka salama machungu ya mlipuko wa bandari ya Beirut kwa subira na uvumilivu.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo Alhamisi katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Lebanon, Michel Aoun. Ametoa mkono wa pole na salamu za rambirambi kwa serikali na taifa la Lebanon na kusema: Tukio la mlipuko wa bandari ya Beirut limewatia huzuni na simanzi Wairani, na wananchi wote hapa nchini wanashirikiana na wenzao wa Lebanon katika msiba huu.

3472203

captcha