IQNA

Jasusi wa zamani wa Saudia awekewa walinzi Canada baada ya vitisho vya MBS

22:00 - August 09, 2020
Habari ID: 3473049
TEHRAN (IQNA)- Serikali ya Canada imeongeza walinzi wa Ali Saad al-Jabri, mkuu wa zamani wa Idara ya Ujasusi ya Saudi Arabia ikihofia kuuawa na serikali na Saudi Arabia.

Gazeti la Globe and Mail la Canada limeripoti kuwa, Idara ya Usalama ya nchi hiyo limefichua habari ya kufanyika juhudi mpya za kutaka kumuua Saad al-Jabri na ndio maana serikali ya nchi hiyo imechukua uamuzi wa kushadidisha ulinzi na usalama mahala anapoishi.

Ripoti zinasema kuwa, mahala anapoishi Saad al-Jabrhi hivi sasa pana ulinzi mkali ambapo mbali na walinzi wake binafsi kuna sakria usalama wa serikali ya Canada ambao wamepewa jukumu la kumlinda mkuu huyo wa zamani wa Idara ya Intelijensia la Saudi Arabia.

Wiki iliyopita Saad al-Jabri, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Canada na anayejulikana kama "Kisanduku Cheusi cha Aal Saud" aliwasilisha mashtaka katika mahakama moja ya Marekani akisema kuwa, Muhammad bin Salman maarufu kama MBS mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia mwaka 2018 alituma timu ya kumuua, ingawa njama za mauaji hayo zilisambaratishwa na viongozi wa Canada.

Saad al-Jabri ana nyaraka muhimu zinazomhusu mfalme Salman bin Abdul-Aziz pamoja na mwanawe Muhammad bin Salman ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo ambapo kama nyaraka hizo zitavuja na kusambazwa zinaweza kuharibu mno haiba ya bin Salman ulimwenguni.

Itakumbukwa kuwa, Jamal Khashoggi, mwandishi habari wa Kisaudia wa gazeti la Washington Post aliuawa kinyama mwaka 2018 kwa amri ya mrithi huyo wa kiti cha ufalme. Khashoggi aliuawa kikatili katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul Uturuki na mwili wake kukatwa vipande vipande.

3472221

captcha