IQNA

Magaidi wateka wanafunzi wengine 80 Waislamu nchini Nigeria

17:07 - June 18, 2021
Habari ID: 3474018
TEHRAN (IQNA)- Zaidi ya wanafunzi 80 Waislamu nchini Nigeria wametekwa nyara katika shambulizi la watu waliokuwa na silaha huko Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo inayokumbwa na ukosefu wa usalama.

Polisi ya Nigeria imetangaza kuwa, shambulizi hilo lilifanyika Alkhamisi ya jana dhidi ya shule moja ya mji wa Birnin Yauri kwenye jimbo la Kebbi na kwamba zaidi ya wanafunzi 80 wametekwa nyara.

Shambulio hilo ni la tatu la magenge yenye silaha dhidi ya shule na vyuo nchini Nigeria katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja. 

Mwalimu Usman Aliyu wa shule hiyo, amesema watu hao waliokuwa na silaha walichukua mateka zaidi ya wanafunzi 80, wengi wao wakiwa wasichana.

Amesema waasi hao wamemuua afisa wa polisi, kisha wakavunja lango na kwenda moja kwa moja kwenye madarasa ya wanafunzi.

Msemaji wa polisi katika jimbo la Kebbi, Nafiu Abubakar, amesema afisa huyo wa polisi aliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa makabiliano baina ya wahalifu hao na polisi na kwamba mwanafunzi mmoja pia amejeruhiwa kwa risasi na anaendelea kupata matibabu. 

Zaidi ya watoto na wanafunzi 700 wametekwa nyara na magenge ya waasi nchini Nigeria tangu Desemba.

Mapema mwezii huu familia za wanafunzi waliotekwa nyara na magenge ya wahalifu nchini Nigeria na vilevile jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu zimeitaka serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua madhubuti za kukomboa karibu wanafunzi 200 wa shule moja ya Kiislamu waliotekwa nyara na magenge ya wahalifu katikati mwa Nigeria. Wanafunzi wasiopungua 136 wa Shule ya Kiislamu ya Salihu Tanko walitekwa nyara katika hujuma hiyo kwenye mji wa Tegina.

3978340

captcha