Siku ya Alhamisi CAIR ilifanikiwa kupata hukumu ya jaji wa Mahakama ya Federali ambaye ametaka wakuu wa Gereza la Anchorage kuacha kuwapa wafungwa Waislamu nyama ya nugurwe.
Katika taarifa, CAIR imesema gereza hilo limekiuka taratibu za magereza na katiba kwa kuwalisha Waislamu nyama ambayo imeharamishwa kwa mujibu wa mafundishyo ya Uislamu.
Waislamu katika mji wa Anchorage jimboni Alaska wanafunga saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa masaa 18 ambapo mbali na kulazimishwa kula nyama ya nguruwe pia wanapewa lishe duni sana wakati wa futari na daku. CAIR imesema katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani Waislamu wanapewa mlo wenye kalori 1,100 kwa siku ambao ni chini ya kiwango cha kila siku kilichopendekezwa na wataalamu cha kalori 2,500 kwa wanaume.
CAIR inasema tokea Donald Trump achaguliwe kuwa rais wa Marekani, Waislamu nchini humo wameshuhudia ongezeko kubwa la ubaguzi dhidi yao huku wakishambuliwa na kubugudhiwa na watu wenye chuki dhidi ya Uislamu.