IQNA

Aliyekuwa Waziri wa Utamaduni wa Tunisia aangazia Sifa za Tafsiri ya Qur'ani ya Ibn Ashur

21:52 - January 07, 2024
Habari ID: 3478164
IQNA - Waziri wa zamani wa utamaduni wa Tunisia alibainisha kuwa Tafsiri ya Qur’ani ya Sheikh Muhammad al-Ṭahir ibn Ashur (1879-1973) ilikuwa ni tafsiri ya kwanza ya Qur’ani nzima katika eneo la Kiarabu la Maghreb.

Mohammad al-Aziz ibn Ashur, mjukuu wa marehemu mfasiri wa Qur'ani, aliyasema hayo katika kongamano la kimataifa la Qur'ani lililofanyika Jumamosi mjini Tehran.

Alisema tafsiri hiyo ambayo ina  dibaji 10, inawasaidia sana wanaofanya tafiti za tafsiri ya Quran.

Amesema Muhammad al-Ṭahir ibn Ashur alizaliwa katika familia ya kidini ambayo wengi wao walikuwa wanazuoni na walimu wa Qur’an, na baada ya kumaliza elimu yake, alianza kufundisha Fiqh, Hadith na tafsiri ya Qur'ani katika Chuo Kikuu cha Ez-Zitouna.

Kwa mujibu wa al-Aziz, jina la tafsiri ya al-Tahir ni Tafsir al-Tahrir wa'l-Tanwir na katika moja ya dibaji zake, anaelezea kuhusu tofauti kati ya Tafsir na Ta'weel.

"Pia alitilia maanani sana miujiza ya Qur’ani Tukufu, suala ambalo wafasiri wa Qur'ani waliotangulia hawakulitilia maanani sana."

Sifa nyingine tafsiri hii ya Qur’ani Tukufu ni kufafanua juu ya Asbab al-Nuzul (sababu au matukio ya kuteremshwa).

Kongamano hilo la Qur'ani lililopewa jina la Risalat Allah (Ujumbe wa Mwenyezi Mungu) lilifanyika na Jumuiya ya Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu (ICRO) katika Kitivo cha Theolojia cha Chuo Kikuu cha Tehran mnamo Jumamosi, Januari 6.

Ilikuwa na lengo la kuendeleza na kuimarisha diplomasia ya Qur'ani.

Wasomi wa Kiislamu, wanafikra na wasomi na wawakilishi wa vituo vya Qur'ani kutoka nchi kadhaa zikiwemo Tunisia, Misri, Iraq, Russia, Lebanon, Malaysia, Senegal, Thailand, India na Pakistan walishiriki katika mkutano huo.

3486710

captcha