IQNA

Wabaguzi Uingereza watumia corona kueneza chuki dhidi ya Waislamu

13:15 - April 06, 2020
Habari ID: 3472640
TEHRAN (IQNA) – Makundi ya wabaguzi wenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia yanatumia janga la ugonjwa wa COVID-19 au corona kueneza chuki dhidi ya Waislamu nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa taasisi ya Tell Mama, ambayo hufuatilia vitendo vya ubaguzi dhidi ya Waislamu Uingereza, katika mwezi wa Machi, kuliripotiwa makumi ya matukio ya makundi ya wabaguzi wenye misimamo mikali wakijaribu kuwatuhumu Waislamu nchini Uingereza kuwa wanahusika katika kueneza ugonjwa wa COVID-19.

Taasisi hiyo imesema imelazimika kuweka mambo wazi baada ya kuenea taarifa katika mitandao ya kijami kuwa Waislamu wanakiuka sheria za karantini na wanaendelea kuswali misikitini. Tell Mama imesema  Waislamu wameshambuliwa mara kadhaa na wafuasi wa makundi hayo ya wabaguzi.

Kwa mfano, mfuasi maarufu wa ile itikadi  ubora wa wazungu kuliko wanadamu wengine wote (White Supremacy), alidai katika ukurasa wake wa Twitter kuwa Waislamu wamekusanyika katika msikiti eneo la Wembley na wanakiuka sheria ya karantini. Baada ya uchunguzi ilibainika kuwa madai hayo si kweli na baada ya malalamiko, Twitter ilifuta ujumbe huo.  Aidha kundi la wabaguzi wenye misimamo mikali la English Defense League nalo pia lilidai kuwa Waislamu wanajumuika katika msikiti wa siri mjini Birmingham. Baadaye ilibainika kuwa madai hayo pia yahana msingi.

Mkurugenzi wa Tell Mama, Iman Atta anasema wabaguzi wenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia wanatumia janga la corona kueneza chuku dhidi ya Waislamu na kuwalaumu kuwa wanahusika katika kueneza ugonjwa huo hatari.  Hadi sasa watu 47,806 wameabukizwa corona nchini Uingereza huku wengine 4,932 wakipoteza maisha kutokana an ugonjwa huo.

Aidha Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amelazwa hospitali kutokana na kutopungua dalili za maambukizi ya COVID-19 aliyopata tangu alipobainika kukumbwa na kirusi hicho siku 10 zilizopita.

3471046

captcha