IQNA

Iran na Afrika

Iran inazingatia kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na Afrika

22:10 - August 25, 2022
Habari ID: 3475680
TEHRAN(IQNA)-Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyeko ziarani nchini Tanzania amesema kuwa, bara la Afrika ni moja ya vipaumbele vikuu vya diplomasia ya kiuchumi ya Iran.

Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo leo jijini Dar es Salaam katika kikao cha wanaharakati wa masuala ya kiuchumi na biashara wa Iran na Tanzania ambapo sambamba na kuashiria uwezo wa kiuchumi, kiviwanda na teklojia wa Iran amesisitiza kuwa, Tehran inatoa kipaumbele katika siasa zake za kigeni kuhusu kustawisha uhusiano wa kiuchumi na mataifa ya Kiafrika hususna Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameitaja Tanzania kama moja ya nchi muhimu barani Afrika ambayo daima imekuwa na nafasi muhimu katika siasa za kigeni za Tehran na kwamba, wananchi na viongozi wa nchi mbili wana mtazamo chanya baina yao.

Abdollahian ameongeza kuwa, kufanyika kikao cha pamoja cha wanaharakati wa masuala ya kiuchumi na kibiashara wa pande mbili ni ushahidi wa wazi wa hamu na shauku ya pande mbili ya kuinua kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi na kwamba, Tanzania ina mazingira mwafaka kwa ajili ya uwekezaji katika sekta mbalimbali kama madini, kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda na utalii.

Kadhalika ameeleza kuwa, kuanzishwa kwa Kamisheni ya Pamoja ya Kiuchumi baina ya Iran na Tanzania kwa minajili ya kufuatilia malengo na mipango na vipaumbele baina ya pande mbili kunaweza kuwa hatua moja muhimu na ya  kianzio kwa ajili ya ushirikiano wenye wigo mpana zaidi.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasili nchini Tanzania Jumatano usiku na kusema kwamba kunatayarishwa ramani ya njia kuhusiana na kuimarisha uhusiano wa Iran na Tanzania ili mchakato huo uchukue mkondo wa kasi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasili katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam nchini Tanzania akitokea Bamako, mji mkuu wa Mali. Punde baada ya kuwasili Amir-Abdollahian alikaribishwa rasmi na Liberata Mulamula, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

https://mfa.gov.ir/portal/NewsView/691167

captcha