IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Iran yalaani kuchomwa moto nakala ya Qur'ani Tukufu Sweden

14:15 - January 22, 2023
Habari ID: 3476444
TEHRAN (IQNA)- Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejiunga na ulimwengu wa Kiislamu katika kulaani vikali kitendo cha kuchomwa moto nakala ya Qur'ani Tukufu nchini Sweden (Usiwidi).

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, kukaririwa kitendo hicho cha kuchomwa moto Kitabu Kitukufu cha Waislamu ni mfano mwingine wa chuki dhidi ya Uislamu, na njama za kuchochea ghasia miongoni mwa wafuasi zaidi ya bilioni 1.5 wa dini hiyo tukufu.

Hii ni baada ya baada ya kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia na mwenye chuki dhidi ya Uislamu wa Denmark, Rasmus Paludan, kuchoma moto nakala ya kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani Tukufu nje ya ubalozi wa Uturuki katika mji mkuu Sweden. 

Kan'ani ameeleza bayana kuwa: Kwa bahati mbaya, shakhsia wenye misimamo mikali wanaruhusiwa kufanya wanachotaka katika baadhi ya nchi za Ulaya, kwa kisingizio cha uhuru wa maoni na kujieleza. Njama hizi zinalenga kuchochea chuki dhidi ya matukufu na thamani za Uislamu.

Aidha Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imelaani vikali uafriti huo na kusema, hatua hiyo ya kuchomwa moto Kitabu hicho Kitakatifu cha Waislamu kimeumiza hisia za Waislamu zaidi ya bilioni 1.5 kote duniani, na ni tusi dhidi ya matukufu yao.

Islamabad imesema hatua hiyo haihalalishiki kwa vyovyote, hata kwa kutumia kisingizio cha kipumbavu cha uhuru wa maoni. Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan imebainisha kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kuonyesha msimamo mmoja dhidi ya chuki dhidi ya Uislamu na dini nyinginezo, na matukufu yao.

Kabla ya hapo, Uturuki na Baraza la Ushirikiano wa Kiislamu la Sweden zilitoa taarifa ya kulaani vikali kitendo hicho cha kuchomwa moto Qur'ani Tukufu nje ya ubalozi wa Uturuki jijini Stockholm nchini Sweden.

4116198

captcha