IQNA

Kadhi ya Palestina

Indhari ya OIC kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya mji wa Rafah katika Ukanda wa Gaza

18:30 - February 15, 2024
Habari ID: 3478355
IQNA-Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani mashambulizi yanayoendelea kufanywa na jeshi katili la Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na upanuzi wa mashambulizi ya kiholela ya utawala huo kwenye mji wa Rafah, kusini mwa ukanda huo.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imesema katika taarifa yake kwamba "mashambulizi ya Israel huko Rafah yameua shahidi na kujeruhi mamia ya Wapalestina, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, ikiwa ni ishara kwamba utawala huo haramu umedharau na kupuuza tahadhari ya kimataifa ya matokeo mabaya ya kushambulia mji huo ambao umewapa hifadhi zaidi ya Wapalestina milioni 1.5 na unasumbuliwa na ukosefu wa mahitaji ya kimsingi ya binadamu.”

OIC imeonya juu ya "hatari ya kupanuliwa na kuzidishwa kasi ya mashambulizi ya Israel, ambayo ni mwendelezo wa mauaji ya halaiki, kuzidisha mateso ya binadamu katika Ukanda wa Gaza, na jaribio lisilokubalika la kuwafukuza kwa nguvu watu wa Palestina katika nchi yao."

Taaifa ya jumuiya hiyo kubwa zaidi baada ya Umoja wa Mataifa imesema, yanayofanywa na Israel huko Gaza "ni ukengeukaji wa wazi wa uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambayo iliitaka Israel kuchukua hatua za haraka za kuzuia vitendo vyote vilivyomo katika kifungu cha II cha Mkataba wa Kuzuia na Kutoa Adhabu ya Mauaji ya Kimbari.

Shirika hilo pia limelaani mashambulizi, hujuma na ugaidi uliopangwa unaoendelea kufanywa na makundi ya walowezi wa Kiyahudi wenye itikadi kali wakishirikiana na askari wa utawala wa Israel dhidi ya raia wa Palestina, ardhi yao, mali na maeneo yao matakatifu katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikiwemo Quds Mashariki.

OIC pia imekariri wito wake kwa jamii ya kimataifa, hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wa kutekeleza majukumu yake kuhusu haja ya kusitisha kikamilifu mashambulizi ya Israel na kuhakikisha kwamba, misaada ya kibinadamu inawasilishwa kwa watu wa Gaza bila ya masharti yoyote.

Siku 130 zimepita tangu utawala wa Kizayuni uanzishe mashambulizi ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Ghaza hapo tarehe 7 Oktoba 2023 na mpaka sasa Wapalestina 28,576 wamethibitishwa kuuawa shahidi na 68,291 wameshajeruhiwa kwenye jinai ambazo hazijawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya hivi karibuni. Aghalabu ya waliouawa au kujeruhiwa katika mauaji hayo ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina ni wanawake na watoto wadogo.

3487193

Habari zinazohusiana
captcha