IQNA

Hali ya hatari yarefushwa tena nchini Tunisia, maandamano yaendelea

21:01 - February 19, 2022
Habari ID: 3474947
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Tunisia, Kais Saied, amerufusha muda wa hali ya hatari nchini humo hadi mwishoni mwa huu wa 2022, licha ya maandamano yanayoendelea kufanyika kote nchini humo.

Katiba ya Tunisia inapiga marufuku mgomo au mkusanyiko wowote ambao utatambuliwa kuwa unavuruga utulivu wa umma iwapo hali ya hatari itatangazwa nchini humo. Katika kipindi hicho cha hali ya hatari pia kumbi za sinema zinafungwa na vyombo vya habari vinabanwa na kuwekewa mipaka maalumu. 

Katika wiki za hivi karibuni, maelfu ya wananchi wa Tunisia wamekuwa wakiandamana kupinga maamuzi ya Rais Kais Saied. Tangu Julai 25 mwaka jana, Rais wa Tunisia amechukua maamuzi kadhaa yaliyozusha mivutano ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na kufuta mamlaka ya Bunge, kukomesha kinga ya wabunge, kuvunja Bodi ya Kusimamia Katiba, kufuta kazi serikali na kuvunja Baraza Kuu la Idara ya Mahakama. 

Hatua ya hivi karibuni ya kiongozi huyo wa Tunisia ya kulivunja Baraza Kuu la Mahakama imewakasirisha sana wananchi na vyama vya siasa nchini Tunisia kwa kadiri kwamba, mkuu wa Baraza Kuu la Mahakama la Tunisia ametangaza kuwa, lengo la Saied si kufanya mageuzi, bali ni kukidhibiti chombo hicho kama ilivyokuwa kwa taasisi nyingine. Rais Saeid anadai amechukua hatua hiyo kutokana na kucheleweshwa kutoa hukumu za kesi za ufisadi na ugaidi.  

Maamuzi na hatua za kiongozi huyo wa Tunisia zimechochea hasira na machafuko ya kisiasa na kusababisha mkwamo mkubwa wa kisiasa. Raia na vyama vingi vya Tunisia vinakiona kitendo cha Saeid kuwa ni mapinduzi yenye lengo la kurejesha udikteta nchini humo. Wafuasi wa muungano wa kupinga mapinduzi wakiungwa mkono na chama cha Ennahdha, wamefanya maandamano makubwa  wakitoa nara za kusambaratishwa "Mapinduzi ya Rais Kais Saied."

3477875

Kishikizo: tunisia kais saied
captcha