IQNA

Afrika Kusini yataka Israel ichukuliwe hatua kutokana na kuwabagua Wapalestina

22:02 - February 19, 2022
Habari ID: 3474948
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa, kuna haja ya kuchukuliwa hatua ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, kutokana na jinai na mienendo yake ya ubaguzi wa rangi wa apathaidi.

Naledi Pandor amesema hayo katika hotuba yake Bungeni ambapo pia ameiasa serikali ya nchi yake kupunguza zaidi uhusiano wake wa kidiplomasia na Tel Aviv.

Amebainisha kuwa, historia ya utawala wa zamani wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini (apartheid) inailazimisha nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kuwa sauti ya wanaodhulumiwa na kutelekezwa katika kona mbalimbali za dunia.

Bi Pandor ambaye pia anaongoza jitihada za kusitisha kikamilifu hadhi ya utawala ghasibu wa Israel ya kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika ameongeza kuwa, anatumai Baraza la Mawaziri la nchi hiyo litauchukulia hatua ya moja kwa moja utawala wa Tel Aviv kwa mienendo yake ya apartheid ya kimfumo.

Hivi karibuni, Amnesty International ilikuwa taasisi ya karibuni zaidi ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kuitangaza Israel kuwa ni utawala wa apartheid.

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Afrika Kusini , msimamo wa Pretoria wa kupinga uanachama mtazamaji wa Israel ndani ya Umoja wa Afrika unatokana na Hati ya AU inayopinga ukoloni, ubaguzi, na ukaliaji wa mabavu wa ardhi.

1400112

captcha