IQNA

Ubaguzi wa Israel

Afrika Kusini yataka UN iitambue Israel kuwa ni 'utawala wa apathaidi'

21:08 - July 29, 2022
Habari ID: 3475554
TEHRAN (IQNA)- Afrika Kusini imeelezea wasiwasi wake juu ya ukatili unaoendelea wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina na kwa msingi huo imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuitambua Israel kama taifa la apathaidi au ubaguzi wa rangi.

Akizungumza jana Jumanne katika mkutano wa pili wa Wawakilishi wa Viongozi wa Palestina barani Afrika katika mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria, Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa nchi hiyo, Naledi Pandor, amesema kuwa "matukio ya Palestina yanakumbusha uzoefu wa historia ya Afrika Kusini yenyewe ya ubaguzi wa rangi na ukandamizaji. "

Pandor amesisitiza kwamba mapambano ya Waafrika Kusini wenyewe dhidi ya ubaguzi wa kimfumo ulioidhinishwa na serikali yanawapa uwezo wa kuelewa hali ya watu wa Palestina, na juongeza: "Tulijionea wenyewe athari za kukosekana kwa usawa wa rangi, ubaguzi na kukana na hatuwezi kusimama wakati kizazi cha Wapalestina kimeachwa nyuma."

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyad Al-Maliki akizungumza na Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC) kufuatia kikao hicho, amepongeza wito wa Pandor na kuongeza kuwa: "Ikiwa kuna nchi ambazo zinaweza kuelewa mateso na mapambano ya uhuru na ukombozi wa Palestina, basi ni bara la Afrika na watu wa Afrika."

Kwa muda wa miaka 27 iliyopita, uhusiano kati ya Wapalestina na Afrika Kusini umeimarika na kubakia imara, huku Pretoria mara nyingi ikitoa uungaji mkono kwa kadhia ya Palestina na kulaani uvunjaji sheria wa Israel duniani.
Mwezi uliopita, Afrika Kusini iliitaka jamii ya kimataifa kuiwajibisha Israel kutojana na hali ya kinyama ambayo Wapalestina wamekuwa wakikabiliwa nayo, na mwaka jana ililaani kitendo cha Umoja wa Afrika (AU) cha kutoa hadhi ya mwanachama mwaangalizi kwa Tel Aviv, hatua ambayo ilibatilishwa mapema mwaka huu.

Mwezi Aprili pia shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International liliitaja Israel kuwa utawala wa kibaguzi na kutangaza kuwa, mauaji na mateso yanayofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina na kuwanyima haki zao ni uhalifu na jinai dhidi ya binadamu.

Amnesty International imeandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Ubaguzi wa rangi (apartheid) sio jambo lililopita na la kihistoria tu, bali pia ni ukweli na hakika inayowasumbua kila siku mamilioni ya Wapalestina katika maeneo yao yanayokaliwa kwa mabavu na inaendelea hadi hii leo." 

Waziri huyo ameitolea wito jamii ya kimataifa kuitangaza  Israel kama utawala wa apathaidi au ubaguzi wa rangi, akisema kwamba Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) lazima liunde kamati kuchunguza kadhia hiyo.
Amesisitiza zaidi kwamba msimamo wa serikali ya baada ya ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini kuhusu Palestina "siku zote umekuwa wazi, thabiti na unaoambatana na jamii ya kimataifa."

4073939

Habari zinazohusiana
captcha