IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kuridhia Marekani kwa ajili ya kuepukana na vikwazo ni kosa kubwa na pigo kwa nguvu za kisiasa

20:21 - March 10, 2022
Habari ID: 3475030
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuiridhia Marekani au dola jengine lolote lile kwa ajili ya kuepukana na vikwazo ni kosa kubwa na pigo kwa nguvu za kisiasa.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika mkutano na Mkuu na wajumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu.

Amesema, kuiridhia Marekani au dola jengine lolote lile kwa ajili ya kuepukana na vikwazo ni kosa kubwa na pigo kwa nguvu za kisiasa na akongeza kuwa, hakuna pendekezo la ujuha na uwanagenzi mkubwa zaidi kama la mtu anayesema tupunguze nguvu zetu za kiulinzi ili adui asije akakereka.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kuwa, nguvu na uwezo wa taifa ni suala mchanganyiko na majimui iliyoshikana pamoja; na akalifafanua hilo kwa kusema, "sayansi na teknolojia" na "ufikirivu, ubunifu na uhuru wa kifikra" ni miongoni mwa nguzo zinazoimarisha uwezo wa kitaifa; na kwa hivyo kama hakutakuwepo na uhuru wa kifikra na maendeleo ya kifikra, sayansi na teknolojia haziwezi kuleta ufumbuzi.

Ayatullah Khamenei ametaja "usalama na nguvu za kiulinzi" "uchumi, ustawi wa jamii na hali nzuri za maisha ya watu", "nguvu za kisiasa na uwezo wa kuwa na sauti katika kudhamini maslahi ya taifa katika uga wa kikanda na kimataifa", "utamaduni na mtindo wa maisha", na "mantiki yenye mvuto athirifu katika kuamiliana na mataifa mengine" kuwa ni mihimili mingine ya nguvu za kitaifa na akasisitiza kwamba, kuyavutia mataifa kunaijengea nchi stratejia imara; na hilo ni jambo muhimu sana.

Kiongozi Muadhamu amebainisha kuwa, kama wangesikilizwa watu waliotaka baadhi ya mihimili ya nguvu za taifa ivunjwe, leo Iran ingekabiliwa na hatari kubwa, lakini kwa irada na rehma za Mwenyezi Mungu mapendekezo hayo hayakupata fursa ya kutekelezwa.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei alitaja mifano ya mapendekezo hayo kuwa ni kuacha kujihusisha na masuala ya kikanda ili kutompa kisingizio adui au kuacha kujiendeleza kisayansi katika uga wa nyuklia, mapendekezo ambayo amesema ni pigo kwa nguvu za taifa. Amelifafanua hilo kwa kuhoji: "Kujishughulisha na masuala ya eneo kunatufanya tuwe imara mno kistratejia na kuongeza nguvu zetu za kitaiifa, kwa nini tuachane nako? Maendeleo ya kisayansi ya nyuklia, nayo pia yanahusu uwezo wa kudhamini mahitaji ya nchi katika mustakabali wa karibu, na kama tutaachana nayo, miaka michache baadaye tutanyoosha mkono wa kuomba wapi na kwa nani?"

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesisitiza kwamba, kuwa imara kwa mfumo kunaimarisha nguvu na uwezo wa kitaifa na akafafanua kuwa, nguvu za kitaifa ni kitu muhimu sana kwa kila nchi; na taifa lolote lile linalotaka liwe huru, litukuke, liweze kutumia maliasili zake muhimu kama linavyotaka lenyewe na liweze kusimama imara kukabiliana na matakwa ya wengine, inapasa liwe imara na lenye nguvu.

4041867

captcha