IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kadhia ya Wapalestina ipo hai na inazidi kuimarika na kupata nguvu kila siku

15:38 - April 13, 2022
Habari ID: 3475120
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema licha ya sera na azma ya Marekani na washirika wake ya kutaka kulisambaratisha suala la Palestina, na kuifanya dunia isahau uwepo kwa taifa hilo, lakini kadhia ya Wapalestina ipo hai na inazidi kuimarika na kupata nguvu kila siku.

Ayatullahi Ali Khamenei alisema hayo jana jioni mjini Tehran katika mkutano wake na wakuu wa mihimili mitatu ya serikali ya Iran, kwa mnasaba wa usiku wa 10 wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kueleza kuwa, wananchi wa Palestina bila shaka watapata ushindi wa mwisho kwa Baraka za Allah, kutokana na harakati (za makundi ya muqawama) zinazoendelea.

Hali kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano wake na maafisa wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameihutubu Saudi Arabia kuhusu vita vya Yemen na kusema: "Nina ushauri kwa Wasaudi, na ninautoa kwa nia njema. Kwa nini mnaendeleza vita ambavyo mna uhakika hamuwezi kushinda? Kwa azma, mikakati na moyo wa wananchi wa Yemen na viongozi wao, hakuna uwezekano wowote wa kupata ushindi. Tafuteni njia ya kuondoka kwenye vita hivi."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema changamoto zote zinazolikabili taifa hili zinaweza kupatiwa ufumbuzi na kusisitiza kuwa, Mfumo wa Uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umepata mafanikio mengi katika sekta tofauti na kuwa kivutio kikubwa kwa mataifa mengi duniani.

Ameongeza mafanikio iliyoyapata Jamhuri ya Kiislamu kama vile kuimarika nafasi na ushawishi wa Iran katika eneo, yamelifanya taifa hili liwe kiigizo chema.

Amewataka viongozi na wakuu wa serikali ya Iran kutosubiri matokeo ya mazungumzo ya kuondolewa vikwazo Tehran huko Vienna akisisitiza kuwa, matokeo ya vikao hivyo hayapaswi kuathiri utendaji kazi wa kila siku wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu.

Ayatullah Ali Khamenei amesema mazungumzo ya kujaribu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA yanaendelea vizuri huko Vienna, na kwamba Iran itaendelea kusimama kidete mkabala wa kujitakia makuu upande wa pili wa mazungumzo hayo.

Amesema: Mazungumzo yanaendelea vizuri huko Vienna, lakini Marekani ambayo ilishindwa kufungamana na majukumu yake ndani ya JCPOA, hivi sasa imenasa kwenye kinamasi.

Kiongozi Muadhami amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imefanikiwa kukabiliana na changamoto na matatizo mengi kwa kutegemea wananchi wake, na pia itavuka salama hatua hii.

Amesisitiza kuwa, "ni muhimu sana kutosahau kuwa Wamarekani wenye kiburi walikiri wazi wazi juu ya kufeli na kusambaratika vibaya sera yao ya mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya taifa la Iran."

3478470

captcha