IQNA

Kiongozi Muadhamu apongeza mapambano ya taifa la Iran dhidi ya Uistikbari

10:41 - March 22, 2022
Habari ID: 3475065
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyid Ali Khamenei amesema kuhusu matukio ya dunia yanayoendelea kujiri katika nchi za Afghanistan, Ukraine na Yemen kwamba: "matukio yote haya yanaonyesha ukweli wa taifa la Iran na machaguo sahihi liliyofanya katika kupambana Uistikbari."

Katika hotuba aliyotoa Jumatatu jioni, ambayo ilirushwa hewani mubashara kupitia redio na televisheni, katika siku ya mwanzo ya mwaka mpya wa 1401 Hijria Shamsia, Ayatullah Khamenei ametoa salamu za hongera za kuadhimisha Sikukuu ya Nouruz na kuanza karne mpya, sambamba na kuashiria masuala kadhaa yanayoendelea kujiri hivi sasa duniani; na akasema, masuala yote hayo yanahitaji tadbiri, upigaji hatua, uamuzi na utekelezaji sahihi; na akafafanua kwa kusema: wakati zinapotazamwa kadhia zinazojiri duniani, kinachodhihirika zaidi ni ukweli kwamba taifa la Iran lilichukua hatua sahihi katika kukabiliana na kambi ya Uistikbari.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kuwa, katika kukabiliana na kambi ya Ubeberu na Uistikbari, taifa la Iran lilitumia machaguo ya "kusimama imara, kutosalimu amri, kutokuwa tegemezi, kulinda uhuru wake na kuimarisha upande wa ndani wa Mfumo na nchi" na akaongezea kwa kusema "maamuzi haya yalikuwa ya kitaifa na sahihi."

Ayatullah Khamenei ameendelea kueleza kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu ameliandalia taifa la Iran mazingira ya kuwa na matumaini na akasema: waacheni maadui wakasirishwe na matumaini liliyonayo taifa la Iran.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia matukio ya nchi iliyodhulumiwa na ya Waislamu ya Afghanistan na namna Wamarekani walivyoondoka baada ya miaka 20 ya dhulma na jinai walizotenda; na akasema, yanayojiri Ukraine ni mfano mwingine pia, ambapo rais wa nchi hiyo aliyewekwa madarakani na Wamagharibi sasa anatumia lugha kali kuwahutubu wao Wamagharibi.

Halikadhalika, Ayatullah Khamenei amezungumzia kadhia za Yemen na mashambulio ya kila leo ya makombora na mabomu yanayowaandama wananachi imara wa nchi hiyo; na kwa upande mwingine akaashiria pia hatua ya Saudi Arabia ya kuwakata vichwa vijana na chipukizi 80 wa nchi hiyo na akasema: "kadhia zote hizi zinaonyesha giza lililotanda duniani na mbwamwitu wanyonya damu wanaoidhibiti dunia".

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kudhihirika wazi ubaguzi wa rangi wa Magharibi ni nukta nyingine ya kadhia za Ukraine na akasema: kuwatenganisha watu weusi na weupe na kuwateremsha weusi kwenye treni au kueleza waziwazi Wamagharibi katika vyombo vyao vya habari kwamba wanasikitishwa na kutokea vita Ulaya badala ya Mashariki ya Kati, ni mfano mwingine wa ubaguzi wa rangi ulio dhahiri wa Magharibi.

Mfano mwingine wa undumakuwili wa Ulimwengu wa Magharibi aliouashiria Ayatullah Khameni katika hotuba yake ni namna unavyozichukulia na kuamiliana nazo dhulma na uonevu unaofanywa katika nchi tofauti na akasema: ikiwa dhulma itafanywa katika nchi zinazowatii wao, hawaonyeshi radiamali na hisia yoyote ile; lakini licha ya uonevu na dhulma zote hizi zinazofanywa (na wanazinyamazia) lakini wanadai kutetea haki za binadamu; na kwa kupitia madai hayo ya uongo wanataka kuzirubuni kimabavu nchi zenye misimamo huru.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena kwamba: kipindi hiki katika historia ya zama hizi kimefichua na kuweka wazi zaidi dhulma na ubeberu uliopo; nao walimwengu wanaendelea kujionea moja kwa moja dhulma hizo na undumakuwili huo.

3478252/

captcha